Madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda wanaofanya shughuli zao katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi, wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kulinda maisha yao pamoja na abiria wanaowasafirisha.
Wito huo umetolewa Oktoba 13, 2026, na Sajenti wa Polisi, Veronica Rumisha, wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva hao, akiwahimiza kutumia kofia ngumu (helmet) kila wanapoendesha pikipiki.
Rumisha amesema kuvaa kofia ngumu ni hatua muhimu ya kujikinga na majeraha makubwa ya kichwa yanayoweza kusababishwa na ajali za barabarani.
Vilevile, amewataka madereva hao kuachana na tabia ya kuendesha pikipiki kwa mwendokasi pamoja na kubeba abiria zaidi ya idadi inayoruhusiwa kisheria, hali inayofahamika kwa jina la mshikaki.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa madereva wa bodaboda kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani wakati wote wanapotekeleza majukumu yao ya usafirishaji, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza ajali na kuimarisha usalama kwa watumiaji wote wa barabara.






