Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameitaka menejimenti na watumishi wa wizara hiyo kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi katika utendaji na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unazalisha matokeo yanayoonekana kwa wananchi, kwa kuzingatia mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima ametoa wito huo Oktoba 15, 2026, jijini Arusha, alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa PAPU International Conference Center (PICC).
Amesema huduma za maendeleo na ustawi wa jamii ni msingi muhimu wa kujenga mtaji watu na kuimarisha uwezo wa Taifa, hivyo ni muhimu kwa wizara kuendeleza sera na programu zinazolenga malezi na ulinzi wa mtoto, kuimarisha familia, kuwawezesha wanawake kiuchumi, pamoja na kuboresha ustawi wa wazee na makundi maalum.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuoanisha programu na huduma za wizara na Ajenda ya Jamii 2050 ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na fursa zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Akizungumzia masuala ya utumishi, Dkt. Gwajima ameitaka menejimenti kuweka mazingira bora ya kazi, kuimarisha mashauriano kati ya viongozi na watumishi, na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafanyakazi zinatatuliwa kwa wakati na kwa haki.
Amewahimiza watumishi kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na uadilifu, huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Pia, amesisitiza matumizi yenye tija ya teknolojia, ushirikiano kati ya idara na vitengo, pamoja na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayopima matokeo ya kazi.
Kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri huyo ameelekeza tathmini ya robo ya kwanza kuzingatia si kiwango cha fedha zilizopokelewa na kutumika pekee, bali pia shughuli zilizotekelezwa na manufaa yaliyopatikana kwa wananchi.
Ameagiza taarifa za utekelezaji wa bajeti kuwasilishwa kabla ya mwisho wa Oktoba 2026. Vilevile, ameitaka menejimenti kufuatilia maendeleo ya utekelezaji kila mwezi, kuondoa vikwazo vinavyojitokeza mapema na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa madhumuni yaliyoidhinishwa.






