Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Watanzania wanachangia asilimia 90 ya nguvu kazi inayotekeleza mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Malangali mkoani Rukwa, hatua inayoongeza ushiriki wa wataalamu wa ndani katika miradi mikubwa ya nishati nchini.
Makamba ameyasema hayo Oktoba 15, 2026, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa yote nchini na Gridi ya Taifa na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika.
Aidha, Makamba amebainisha kuwa majaribio ya mitambo ya kituo hicho yanatarajiwa kuanza katikati ya Novemba 2026, hatua itakayokaribisha kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha sekta ya nishati mkoani Rukwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 85.17, huku shughuli za kuwasha na kuingiza umeme kwenye mfumo zikitarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.
Kituo hicho kinajengwa na kampuni ya TBEA kutoka China kwa gharama ya Sh bilioni 161.9. Kitakuwa na uwezo wa kupokea umeme wa kilovolti 400 na kuushusha hadi kilovolti 220, 66 na 33 kwa ajili ya usambazaji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kituo hicho kitakuwa na transfoma nne na njia nane za kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Rukwa.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuvutia uwekezaji, kuchochea ujenzi wa viwanda na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na madini.
Vilevile, mradi huo unatarajiwa kufungua fursa mpya za ajira na biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, huku ukichangia ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.






