Kampuni ya usafiri wa kidijitali ya Bolt imewazawadia madereva wake waliofanya vizuri kwa kuwapatia mafuta ya vyombo vya usafiri, matairi na zawadi nyingine mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutambua mchango wao katika utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Zawadi hizo zimetolewa wakati wa kifungua kinywa kilichoandaliwa na kampuni hiyo kwa ajili ya madereva wake katika ofisi za Bolt jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu Mwandamizi wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, amewashukuru madereva na abiria kwa kuendelea kuamini na kutumia huduma za kampuni hiyo.
Aidha, amewahimiza madereva kuzingatia sheria na kanuni za usafiri, pamoja na kudumisha heshima na ushirikiano wanapotekeleza majukumu yao ili kuhakikisha abiria wanapata huduma salama na zenye ubora.
Katika hatua nyingine, Bolt imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na wadau husika kuwezesha maeneo maalumu ya kupakia na kushusha abiria katikati ya jiji la Dar es Salaam, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri.
Kwa sasa, eneo maalumu la maegesho limetengwa Feri, huku mipango ikiendelea ya kuanzisha maeneo mengine katika maeneo ya Posta na Kariakoo.
Hatua hiyo inatarajiwa kurahisisha shughuli za madereva na abiria, kupunguza changamoto za kupata maeneo ya kupakia na kushusha abiria, na kuboresha uzoefu wa watumiaji wa huduma za Bolt jijini Dar es Salaam.






