BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanga mikopo na ruzuku yenye jumla ya Shilingi bilioni 535.7 kwa wanafunzi 165,775 katika awamu ya kwanza ya mwaka wa masomo 2026/2027.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumamosi, Oktoba 10, 2026, katika ofisi za HESLB zilizopo Tazara Veterinary, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Dkt. Bill Kiwia, amesema mgao huo unawahusu wanafunzi wa shahada ya awali, stashahada, wanaoendelea na masomo pamoja na wanufaika wa Samia Scholarship.
Amesema kati ya wanafunzi hao, 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 246.88, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa mikopo ya Shilingi bilioni 22.9.
Aidha, wanafunzi 873 wa mwaka wa kwanza wanaonufaika na Samia Scholarship wamepangiwa ruzuku ya Shilingi bilioni 4.5.
Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, Dkt. Kiwia amesema wanafunzi 79,115 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 252.4.
Ameongeza kuwa wanafunzi 1,554 wa stashahada wanaoendelea na masomo wamepangiwa mikopo ya Shilingi bilioni 3.8, huku wanafunzi 926 wanaoendelea kunufaika na Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Shilingi bilioni 5.1.
Dkt. Kiwia amesema upangaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata mikopo na ruzuku kwa ajili ya kugharamia masomo yao katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine, amewataka waombaji ambao hawakupangiwa mikopo au ruzuku katika awamu ya kwanza kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanafunzi (SIPA), wakati mchakato wa uchambuzi na upangaji wa awamu zinazofuata ukiendelea.
Amesisitiza kuwa kutopangiwa mkopo au ruzuku katika awamu ya kwanza hakumaanishi kuwa mwombaji amekosa nafasi moja kwa moja, kwani HESLB bado inaendelea na taratibu za uchambuzi na upangaji kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Kwa mwaka huo wa masomo, Serikali imetenga jumla ya Shilingi trilioni 1.06 kwa ajili ya mikopo na ruzuku za wanafunzi wa elimu ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa ya HESLB, fedha hizo zinalenga kugharamia wanafunzi 292,463, wakiwemo wanafunzi 111,342 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali.
Bajeti hiyo pia inajumuisha wanafunzi 24,978 wa stashahada, wakiwemo wanafunzi 14,000 wa mwaka wa kwanza, pamoja na wanafunzi 2,738 wa shahada ya awali wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship, wakiwemo wanufaika wapya 1,000.
Vilevile, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya wanafunzi 513 wa Stashahada ya Juu ya Sheria kwa Vitendo, wakiwemo wanafunzi wapya 350.






