KAMBI ya matibabu ya kibingwa iliyohusisha wataalamu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya Tanzania imewanufaisha wagonjwa zaidi ya 810 nchini Malawi, huku wagonjwa 64 wakifanyiwa upasuaji na wengine 49 kupewa rufaa ya kwenda kupata matibabu zaidi katika hospitali hiyo nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo, Katibu Mkuu wa Utawala wa Wizara ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Malawi, Bestone Chisamile, amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa imeonesha kwa vitendo umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa.
Chisamile amesema ushirikiano wa afya kati ya Tanzania na Malawi umetekelezwa kupitia kambi hiyo, huku nchi hizo zikiendelea na majadiliano ya kuupanua ili kujumuisha huduma za matibabu, mafunzo kwa wataalamu, masuala ya dawa na rufaa za wagonjwa.
Amesema majadiliano hayo yanalenga kutathmini manufaa ya kambi hiyo kwa wagonjwa na kuweka msingi wa kurasimisha ushirikiano mpana zaidi kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, ameeleza kuwa wataalamu wa Tanzania wameleta ujuzi na uzoefu katika fani mbalimbali za matibabu, huku wakipata nafasi ya kubadilishana maarifa na wenzao wa Malawi katika Hospitali ya Mzuzu na Hospitali ya Kamuzu iliyopo Lilongwe.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Agnes Kayola, amesema kambi hiyo imekuwa fursa muhimu kwa wananchi wa Malawi kupata huduma za kibingwa na kwa wataalamu wa afya wa nchi hizo mbili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.
Kayola amesema kati ya wagonjwa zaidi ya 810 walionufaika na huduma zilizotolewa, 64 wamefanyiwa upasuaji na 49 wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unaimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Malawi, hususan katika kuboresha huduma za afya na kuongeza uwezo wa wataalamu wa nchi hizo.
Kambi hiyo iliyoanza Septemba 28, 2026, imehitimishwa kwa ushirikiano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), SOTAC na MSD.
Katika kutoa huduma hizo, timu ya wataalamu imetumia magari maalumu ya kisasa yenye vyumba vya upasuaji, yanayowezesha utoaji wa huduma za matibabu katika mazingira mbalimbali.






