LISSU AHOJI MSINGI WA KISHERIA WA MASHTAKA YANAYOMKABILI
DAR ES SALAAM, Septemba 24, 2026
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo. CHADEMA, Tundu Lissu, leo ameendelea kutoa majumuisho yake ya mwisho (submission) katika kesi ya uhaini inayomkabili mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa hatua hiyo.
Lissu anaendelea kujielekeza zaidi katika hoja za kisheria, akiiomba Mahakama kutathmini kama maneno anayodaiwa kuyasema yanaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda kosa la uhaini analoshtakiwa nalo. Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.
Moja ya hoja kuu alizosisitiza Lissu ni kwamba suala si tu kama alitamka maneno yanayodaiwa na upande wa mashtaka, bali kama maneno hayo yanakidhi vipengele vyote vinavyotakiwa kisheria ili kuthibitisha kosa linalomkabili la uhaini.
Katika majumuisho yake, Lissu pia amehoji namna shtaka lilivyoandaliwa, akisema upande wa mashtaka unadai kuwa alichochea watu kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini haujaainisha kwa uwazi ni sehemu gani ya Serikali au viongozi gani waliodaiwa kutishiwa.
Lissu alihoji ni nani hasa anayodaiwa kuwa alimtishia akirejea uwezekano wa kuwa Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Polisi au viongozi wengine wa Serikali. Hoja hiyo imejengwa katika tafsiri yake kwamba neno Government (serikali) lina maana pana kikatiba na hivyo shtaka linapaswa kubainisha kwa usahihi mhusika au chombo kinachodaiwa kutishiwa.
Lissu pia ameendelea kupinga tafsiri kwamba kauli yake ya kutaka kuzuia uchaguzi yenyewe inaweza kuwa msingi wa kosa la jinai linalomkabili. Katika hoja alizowasilisha siku ya kwanza, alisema kwamba kuzuia uchaguzi kama lengo lililotajwa hakutambuliwi kama lengo linalounda kosa chini ya kifungu cha sheria kinachotumika katika shtaka lake, hoja ambayo ameendelea kuifafanua katika majumuisho yake leo.






