MEYA wa Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, Dkt. Nicas Mawazo, amewataka wawekezaji waliopo katika manispaa hiyo kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za kijamii, hususan miundombinu ya elimu, ili kuchochea maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo yao ya uwekezaji.
Dkt. Mawazo ametoa wito huo wakati wa ziara ya kutembelea viwanda vya Qounquer Investment Company Ltd, kinachozalisha tishu, na Ufresh Food Ltd, kinachozalisha juisi, vilivyopo Kata ya Kongowe, ambapo ameeleza kuwa baadhi ya shule, ikiwemo Sekondari ya Mwambisi, zinakabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Amesema pamoja na Serikali kuendelea kutekeleza wajibu wake katika kuboresha sekta ya elimu, wazazi, walezi, jamii na wawekezaji wana nafasi muhimu ya kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
“Serikali inatekeleza sehemu yake, jamii, wazazi na walezi nao wanapaswa kuchangia. Wawekezaji wanapaswa kurudisha kwa jamii kwa kusaidia shughuli za maendeleo na kuboresha miundombinu ya elimu,” amesema Dkt. Mawazo.
Aidha, amewataka watendaji na wenyeviti wa mitaa na kata kusimamia ipasavyo usafi wa mazingira, huku akizisisitiza kampuni na viwanda kuhakikisha vina mifumo bora ya maji taka ili kuzuia uchafuzi wa mazingira na kero kwa wakazi wa maeneo jirani.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko na Mahusiano wa Qounquer Investment Company Ltd, Robert Baclay, amesema kiwanda hicho kinachangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Mwambisi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Baclay amesema kampuni hiyo pia ina mpango wa kushughulikia changamoto zinazohusiana na mfumo wa maji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka kiwanda hicho.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kinapanga kuachana na matumizi ya kuni na kuhamia katika matumizi ya nishati safi, hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Akizungumzia changamoto ya maji yanayotoka kiwandani, mkazi wa eneo hilo, Samwel Raphael, amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo bora ya maji taka ili kuzuia maji hayo kusambaa katika maeneo ya makazi na kuwasababishia usumbufu wananchi.
Naye Mdhibiti Ubora wa Ufresh Food Ltd, Noela Ngusa, amesema kampuni hiyo iliwahi kukabiliwa na changamoto katika mfumo wa maji taka na matibabu yake, lakini imefanya marekebisho ili kuhakikisha maji yanatibiwa kabla ya kutolewa nje ya kiwanda.
Ngusa amesema kampuni hiyo pia inachangia mabati 500 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Mwambisi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kusaidia kuboresha mazingira ya elimu katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, Byson Mpogoza, amezitaka kampuni na viwanda kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sura ya 191, pamoja na kanuni zinazolenga kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Mpogoza amesema kifungu cha 144 cha sheria hiyo kinahusu masuala ya viwango vya utoaji wa maji taka katika vyanzo vya maji, hatua za kuyatibu kabla ya kuyaingiza katika mifumo ya majitaka na masharti yanayotakiwa kuzingatiwa na viwanda kabla ya kuyaachia maji hayo katika mazingira.
Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa sheria na taratibu za mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na kuhakikisha shughuli za viwanda zinafanyika bila kuathiri mazingira yanayovizunguka.






