Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amekagua maendeleo ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Tagamenda mkoani Iringa hadi Sumbawanga mkoani Rukwa, pamoja na kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Malangali.
Mradi huo wa Tanzania na Zambia (TAZA) unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kupanua muunganisho wa maeneo mbalimbali nchini kupitia gridi ya taifa.
Akizungumza na wananchi baada ya ziara hiyo, Ndejembi alisema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Rukwa kuunganishwa na gridi ya taifa, jambo litakalofungua milango ya uwekezaji katika sekta ya viwanda na kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana.
Alisisitiza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea shughuli za kiuchumi na kuwapa wananchi pamoja na wawekezaji fursa mpya za kujikwamua kiuchumi. Aliwahimiza wananchi kujiandaa kutumia fursa zitakazotokana na kukamilika kwa mradi huo.
“Nimeelezwa hapa mnapokea kilovoti 66, wakati kinajengwa kituo cha kilovoti 400. Umeme huu utasafirisha megawati 600 na utaunganisha vituo saba, huku mikoa ya Kigoma na Katavi nayo ikiunganishwa na gridi hii ya taifa. Tuchangamkie fursa za uwekezaji, umeme huu utamgusa kila mtu,” alisema Ndejembi.
Vilevile, Makamu wa Rais aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu inayojengwa ili iendelee kutoa huduma kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alisema wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa miundombinu hiyo inayotekelezwa chini ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na kujiandaa kupokea uwekezaji mkubwa unaotarajiwa kufanyika mkoani Rukwa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, alisema mradi huo una thamani ya Sh trilioni mbili na umefikia asilimia 90 ya utekelezaji wake.
Alieleza kuwa ujenzi ulianza Novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026.
Twange alisema kwa sasa mkoa wa Rukwa unapata megawati 16 za umeme, wakati mahitaji yake yanafikia megawati 30, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa nishati hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alisema kuwa pamoja na utekelezaji wa baadhi ya miradi ya nishati kufanywa na kampuni za kigeni, asilimia 90 ya vijana wanaofanya kazi katika miradi ya TANESCO ni Watanzania.
Aidha, alisema katika kuendeleza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za ajira 1,400 kwa vijana, ambazo maombi yake yanapatikana kupitia mfumo wa Ajira Portal.
Naye Diwani wa Kata ya Malangali, Andrew Matanila, akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kata hiyo, aliishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo akieleza kuwa umewapatia vijana wengi wa eneo hilo ajira na kuwawezesha kupata kipato cha kukidhi mahitaji yao.
Matanila pia aliishukuru Serikali kwa kuwalipa fidia wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.






