Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya TANESCO na Benki ya CRDB utasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa mijini na vijijini.
Mhe. Ndejembi amesema mpango huo utawawezesha wananchi kupata huduma ya umeme kwa urahisi na kwa wakati, hivyo kuongeza fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza leo, Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini na uzinduzi wa mpango huo, Ndejembi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Misheni 300 unaolenga kuhakikisha hadi mwaka 2030 wananchi milioni 300 barani Afrika wanafikiwa na nishati ya umeme.
Amesema kupitia ushirikiano huo, wananchi wanaostahili watanufaika na utaratibu wa kugharamiwa gharama za uunganishaji wa umeme, hatua inayolenga kuongeza kasi ya kuzifikia kaya takribani milioni 1.7 kwa mwaka, ikiwa sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Nishati.
Ndejembi ameipongeza TANESCO na Benki ya CRDB kwa kuanzisha ushirikiano huo, akisema ni mfano wa namna taasisi za umma na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa tathmini ya mara kwa mara ili kubaini matokeo ya mpango huo na kuhakikisha unaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.






