Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kutoa huduma na ushauri kwa wateja katika mradi wa Kawe 711 jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 16, 2026.
Akizungumza na wateja waliotembelea mradi huo, Afisa Uhusiano wa NHC, Getrude Mallya, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuwapa wananchi fursa ya kujionea nyumba zinazojengwa na shirika hilo, kupata maelezo kuhusu mauzo pamoja na kufahamu taratibu mbalimbali za kumiliki makazi.
Mallya amesema nyumba za NHC zimejengwa kwa kuzingatia ubora na mahitaji ya makazi ya kisasa, huku wateja wakipewa nafasi ya kuchagua nyumba zinazolingana na mahitaji yao na uwezo wao wa kifedha.
Ameongeza kuwa wananchi wanaweza kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na benki zinazoshirikiana na NHC ili kurahisisha upatikanaji wa nyumba, kwa kuzingatia masharti na taratibu za mikopo husika.
Kutokana na fursa hizo, amewahimiza wananchi kutembelea mradi wa Kawe 711 ili kupata taarifa sahihi kuhusu nyumba zinazouzwa na njia zinazoweza kuwawezesha kumiliki makazi bora na ya kisasa.
Kwa upande wao, baadhi ya wateja waliotembelea mradi huo wameipongeza NHC kwa kuwapa nafasi ya kujionea nyumba hizo na kupata ufafanuzi kuhusu ubora wake pamoja na utaratibu wa ununuzi.
Baadhi ya wateja hao wameeleza kuwa taarifa walizopata zimewaongezea uelewa kuhusu fursa za kumiliki nyumba, huku wakitaja nia ya kuendelea na hatua za ununuzi baada ya kuridhishwa na maelezo na huduma walizopatiwa.






