Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amewahimiza wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumpokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anayetarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani humo Oktoba 16, 2026.
Ziara hiyo itajikita katika kukagua miradi ya uwekezaji na maendeleo, pamoja na kufanya mazungumzo na wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maisha na maendeleo yao.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu anatarajiwa kutembelea kongani ya uwekezaji ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), iliyopo Zinga, Wilaya ya Bagamoyo, ambako atakagua shughuli za uwekezaji na maendeleo ya ujenzi wa viwanda.
Baada ya hapo, anatarajiwa kuelekea Mbegani kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kabla ya kukutana na kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo, wilayani humo.
Ziara hiyo inalenga kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya uwekezaji na maendeleo mkoani Pwani, pamoja na kutoa nafasi kwa wananchi kueleza maoni yao na kuwasilisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa Serikali.






