Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga, amezindua awamu ya pili ya kampeni ya PikaSmart mkoani Kagera, inayolenga kuhamasisha wananchi kutumia umeme kama nishati safi, salama na nafuu ya kupikia.
Uzinduzi huo umefanyika kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nyamahanga alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kitaifa inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na umuhimu wake katika kulinda afya za wananchi, kupunguza gharama za kaya, kuhifadhi mazingira na kuokoa muda unaotumika katika shughuli za kila siku.
Alisema Mkoa wa Kagera unaendelea kuunga mkono ajenda hiyo kwa kuhamasisha kaya na taasisi zinazohudumia watu wengi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyamahanga, juhudi za Serikali na Wizara ya Nishati za kuunganisha vijiji vyote vya mkoa huo na huduma ya umeme zimeweka msingi mzuri wa kuwawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika shughuli za kupikia.
Alibainisha kuwa tangu kuanza kwa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, zaidi ya taasisi 80 zinazohudumia watu wengi zimeanza kutumia nishati hiyo, hatua inayosaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Aliongeza kuwa kampeni ya PikaSmart inatarajiwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya umeme kupikia na kuchangia kufanikisha azma ya Serikali ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Dkt. Nyamahanga alisisitiza kuwa Serikali inataka wananchi wanufaike zaidi na miundombinu ya umeme iliyowekezwa, kwa kuitumia si kwa ajili ya mwanga pekee, bali pia katika maandalizi ya chakula.
Alisema matumizi ya majiko ya umeme yanaweza kupunguza moshi ndani ya nyumba na hivyo kulinda afya za wanawake, watoto na watu wengine dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji. Vilevile, yanaweza kupunguza gharama zinazotumika kununua kuni na mkaa.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, aliwataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wengine kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya umeme kupikia inawafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji. Pia aliwasisitiza viongozi hao kutoa mwongozo kuhusu matumizi sahihi na salama ya majiko ya umeme.
Kwa upande wake, balozi wa kampeni hiyo kutoka Tanzania House of Talent (THT), Mrisho Mpoto, alisema PikaSmart inatekelezwa kwa ushirikiano na Serikali, huku ufadhili ukitolewa kupitia mradi wa Modern Energy Cooking Services (MECS) unaohusishwa na Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza.
Alieleza kuwa kampeni hiyo inatekelezwa na THT Innovation Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mpoto alisema kampeni hiyo itafanyika katika mikoa saba nchini, ikihusisha mikutano ya uhamasishaji na maonesho ya vifaa vya kupikia vinavyotumia umeme.
Aliongeza kuwa wananchi watapata fursa ya kujifunza kuhusu vifaa hivyo na kuvipata kwa gharama nafuu kupitia mifumo inayowawezesha kulipa kwa awamu.
Naye Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Liian Mungai, alisema shirika hilo linaunga mkono kampeni hiyo kupitia mpango wa On-Bill Financing, unaomwezesha mteja kupata jiko la umeme na kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia manunuzi ya umeme wa LUKU hadi deni litakapokamilika.
Mungai alisema gharama za awali za kununua majiko ya umeme zimekuwa mojawapo ya changamoto zinazowazuia baadhi ya wananchi kuanza kutumia nishati hiyo, hivyo mpango huo unalenga kupunguza kikwazo hicho.
Aliwahimiza wananchi wa Kagera kutembelea ofisi za TANESCO kwa maelezo zaidi kuhusu masharti ya kujiunga na mpango huo.
Alisisitiza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya umeme kupikia kutasaidia kupunguza ukataji wa miti, kuhifadhi mazingira na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.







