Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS), Richard Kayombo, amezitaka mamlaka za elimu kuanza mapema maandalizi ya madarasa na miundombinu mingine ya shule za sekondari ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2028.
Kayombo ameyasema hayo wakati akifunga mkutano wa uchaguzi mdogo wa kumchagua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT) wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), akisisitiza kuwa maandalizi ya mapema yatasaidia kuhakikisha shule zinakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi wote watakaohitaji kuendelea na elimu ya sekondari.
Amesema hitaji hilo linatokana na mpango wa kuwapokea wanafunzi wanaomaliza Darasa la Sita na Darasa la Saba katika Kidato cha Kwanza kwa pamoja mwaka 2028, hali inayohitaji maandalizi ya kutosha ya madarasa na huduma nyingine muhimu za shule.
Katika hatua nyingine, Kayombo amewahimiza walimu wenye ulemavu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini, akibainisha kuwa hali hiyo haipaswi kuwa kikwazo katika kufikia malengo yao ya kitaaluma na kutoa mchango wao katika maendeleo ya sekta ya elimu.
Amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za walimu, ikiwemo kuongeza ajira, kupandisha madaraja na kulipa stahiki zao, huku akiwataka wahusika kuhakikisha madai ya walimu ambao bado hawajapata haki zao yanafuatiliwa na kutatuliwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Ameeleza kuwa walimu wana nafasi muhimu katika maendeleo ya taifa kwa kuwa wanahusika katika kuandaa wataalamu na viongozi wa sekta mbalimbali.
“CWT ni chama kikubwa kinachotambulika, na kundi hili la walimu ni hazina katika Taifa kwa kuwa lina nafasi kubwa katika kujenga Taifa kutokana na mchango wao katika kuzalisha wataalamu na viongozi kwenye sekta mbalimbali,” amesema Kayombo.
Aidha, amewaelekeza maofisa elimu kuhakikisha upandishaji wa madaraja ya walimu unafanyika kwa haki na kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa, akisisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zinazoweza kuathiri ustawi wao kazini.
Vilevile, amewataka walimu kushiriki katika kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu namna ya kujikinga na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, ili kuwajengea uelewa wa kuchukua tahadhari zinazofaa wakati wa mvua hizo.
Kwa upande wake, Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Suzan Shesha, amesema mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa, ambapo jumla ya kura 37 zilipigwa.
Amesema Mwita Magige alichaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya kupata kura 20, akifuatiwa na Abdalrahmani Ahmadi aliyepata kura 16, huku kura moja ikiharibika.
Shesha ameeleza kuwa Mkoa wa Pwani una walimu takribani 11,000, huku akimuomba Katibu Tawala huyo kusimamia uendeshaji wa mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati ili kuimarisha mawasiliano, ushirikiano na utatuzi wa changamoto zinazowakabili walimu.
Naye Mwita Magige, aliyechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya CWT, amewashukuru wanachama kwa kumchagua na kuhimiza kuendelezwa kwa umoja na mshikamano miongoni mwa walimu.
Ameahidi kuwasilisha changamoto za walimu katika ngazi husika za uongozi wa chama ili ziweze kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi.






