Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martin Shigela, amefanya ziara katika Wilaya ya Mbulu Septemba 24, 2026, kwa ajili ya kukagua maeneo hatarishi yanayoweza kuathiri miundombinu muhimu kutokana na mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwanzoni mwa Oktoba.
Katika ziara hiyo, Shigela ametembelea Bwawa la Dongobesh lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, ambapo njia za kupitisha maji zimepasuka na kusababisha kutokea kwa makorongo makubwa, hali inayohatarisha kingo za bwawa hilo.
Baada ya kukagua eneo hilo na kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi, Mkuu wa Mkoa amewaagiza wahandisi wa Tume ya Umwagiliaji Mkoa wa Manyara, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kufanya tathmini ya haraka ya hali ya bwawa hilo.
Shigela ameagiza tathmini hiyo ikamilishwe na mapendekezo kuwasilishwa ifikapo Ijumaa ya wiki hii ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Amesema maagizo hayo ni sehemu ya maandalizi ya Mkoa wa Manyara kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, pamoja na kulinda miundombinu muhimu na usalama wa wananchi.






