SERIKALI imewataka makandarasi wanawake nchini kutumia miradi wanayopewa kama fursa ya kuthibitisha uwezo wao, kujenga uaminifu na kuongeza nafasi ya kupata kandarasi kubwa na nyingi zaidi.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, wakati akifungua Kongamano la Sita la Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA), lililofanyika jijini Dar es Salaam kwa kaulimbiu isemayo “Wezesha, Jenga, Stawi.”
Kadogosa amesema makandarasi wanawake wanapaswa kutekeleza miradi wanayopewa kwa kuzingatia ubora, weledi na viwango vinavyotakiwa ili kujenga imani kwa wateja na kujiongezea fursa za kushiriki katika miradi mingine mikubwa.
“Hakikisheni kazi ndogo mnazozipata mnazitumia kama fursa ya kupata kazi zaidi. Onesheni uwezo wenu. Taifa linahitaji wanawake wenye uwezo wanaopewa nafasi na kutekeleza kazi kama inavyotakiwa,” amesema Kadogosa.
Amesema Serikali, kupitia Sekta ya Ujenzi, inalenga kuwaona wanawake wakishiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwa waajiri, makandarasi, wamiliki wa kampuni, wataalamu na wabunifu katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Kadogosa amewapongeza makandarasi wanawake kwa mchango wao katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi, ikiwemo mradi wa barabara ya lami mkoani Songwe ulioshirikisha kampuni zaidi ya 15.
Amesema kutokana na juhudi zinazofanywa na makandarasi hao, Serikali imeongeza kiwango cha malipo ya awali kutoka asilimia 15 hadi asilimia 30, hatua inayolenga kuwasaidia katika utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amesema wizara hiyo, kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), itaendelea kukiunga mkono chama hicho kwa kuhakikisha makandarasi wanawake wanapata fursa za kukuza uwezo wao kitaaluma na kibiashara.
Amour amesema msaada huo utajumuisha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo ili kuwawezesha makandarasi wanawake kushindana na kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi.
Naye Rais wa TWCA, Judith Odunga, ameishukuru Serikali kwa kukipa kipaumbele chama hicho na kuwawezesha makandarasi wanawake kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 20 mkoani Songwe.
Odunga amesema Serikali pia imewawezesha kupata mafunzo ya usimamizi wa fedha na miradi, ambayo ni muhimu katika kuimarisha utendaji na ukuaji wa biashara zao.
Kongamano hilo la sita limewakutanisha makandarasi wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili maendeleo ya sekta ya ujenzi, changamoto zinazowakabili na namna ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.






