Shirika la Revival Education Trust limeweka mpango wa kuwawezesha wanafunzi 100 kutoka familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi kurejea shuleni mwaka ujao, kwa lengo la kuwapa nafasi ya kuendelea na elimu na kufikia malengo yao ya maisha.
Akizungumza katika mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful, mwanzilishi wa shule hiyo na msimamizi wa shirika hilo, Diodorus Tabaro, amesema mpango huo utawalenga wanafunzi walioacha masomo kutokana na ukosefu wa fedha, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya vizuri kitaaluma.
Tabaro amesema kati ya wanafunzi 100 watakaonufaika na mpango huo, 50 watapata nafasi za bweni, huku wengine 50 wakisoma bila kuishi shuleni, hatua inayolenga kuzingatia mahitaji na mazingira ya kila mwanafunzi.
Ameeleza kuwa mpango huo unaakisi dhamira ya Revival Education Trust ya kuhakikisha watoto kutoka familia zenye uhitaji wanapata fursa ya elimu, akisisitiza kuwa hali ngumu ya kiuchumi haipaswi kuwanyima wanafunzi nafasi ya kutimiza ndoto zao.
Aidha, Tabaro amesema ana mpango wa kugharamia elimu ya watoto saba katika mwaka wa masomo ujao, huku akiwahimiza watu wenye uwezo wa kifedha kujitokeza na kusaidia wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto zinazowazuia kuendelea na masomo.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali ni muhimu katika kupanua fursa za elimu kwa watoto wenye uhitaji na kuwawezesha kujenga maisha bora ya baadaye.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Can Tanzania, Sixbert Mwanga, ameahidi kuchangia jumla ya Sh milioni 10 kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kupitia Revival Education Trust, inayosimamiwa na Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful.
Mwanga amesema mchango huo unalenga kuwasaidia wanafunzi kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi kupata fursa ya kuendelea na masomo yao.
Ameeleza kuwa uzoefu wake katika safari ya elimu ulimfanya kutambua umuhimu wa msaada kwa wanafunzi wenye uhitaji, akibainisha kuwa baadhi yao hushindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu za kifamilia, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya vizuri darasani.
Amesema baadhi ya wanafunzi hukumbana na vikwazo vya kielimu kutokana na kutofaulu mitihani au kukosa fedha za kulipia mahitaji ya shule, huku wengine wakifanikiwa kuendelea na masomo kwa msaada wa wazazi, ndugu na watu wengine wenye uwezo wa kifedha.
Wakati huo huo, baadhi ya wanafunzi waliohudhuria mahafali hayo wamepongeza mpango wa kuwasaidia wenzao wanaotoka katika familia zenye uhitaji, wakisema utawapa matumaini wale waliokata tamaa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifedha.
Wanafunzi hao wametoa pongezi kwa waanzilishi wa mpango huo, huku wakieleza matumaini yao kuwa jitihada hizo zitasaidia wanafunzi wengi kurejea shuleni na kuendelea na safari yao ya elimu.






