Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, ameipongeza Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) kwa mchango wake katika kusaidia Wizara ya Kilimo kutekeleza majukumu yake, hususan kuimarisha huduma za ugani na kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazoongeza thamani ya mazao.
Silinde ametoa pongezi hizo Oktoba 12, 2026, alipotembelea banda la NAESA katika maadhimisho ya kitaifa kuelekea Siku ya Chakula Duniani, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga.
Katika ziara hiyo, alijionea teknolojia mbalimbali za kilimo, akivutiwa zaidi na mfumo wa uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke (parboiling), unaosaidia kuimarisha punje za mchele na kupunguza kiwango cha kuvunjika wakati wa kusaga.
Amesema teknolojia hiyo ina nafasi muhimu katika kuongeza ubora wa mchele na thamani ya mazao ya wakulima, jambo linaloweza kuongeza mapato yao na kuboresha ustawi wa kiuchumi.
Silinde ameeleza kuwa kuanzishwa kwa NAESA ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Kilimo, hasa katika kuratibu na kusimamia huduma za ugani pamoja na kuhakikisha wakulima wanapata elimu, ushauri wa kitaalamu na teknolojia zinazoweza kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, ameitaka NAESA kuimarisha usimamizi wa huduma za ugani nchini na kuwasilisha taarifa za kila wiki kwa Wizara ya Kilimo kuhusu mwenendo wa shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali.
Amesema taarifa hizo zitasaidia kubaini changamoto zinazowakabili wakulima na kuwezesha Serikali kuchukua hatua kwa wakati, kulingana na mahitaji halisi ya kila eneo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani ya Mazao wa NAESA, Esther Mwaisango, amesema taasisi hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na imejipanga kuimarisha huduma za ugani ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuhakikisha upatikanaji wa chakula unaimarika.
Mwaisango amesema ushiriki wa NAESA katika maadhimisho hayo ulilenga kuonesha teknolojia mbalimbali za usindikaji wa mazao na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna zinavyoweza kutumika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Ameongeza kuwa NAESA inaendelea kuandaa mafunzo kwa maafisa ugani katika halmashauri mbalimbali kuhusu namna ya kutafsiri taarifa za mvua na kuzitumia kutoa ushauri sahihi kwa wakulima, ili kuboresha maamuzi ya kilimo kulingana na hali ya hewa.
Akifafanua kuhusu teknolojia ya uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke, mkufunzi kutoka Chuo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo (MATI Ilonga), kilichopo Kilosa mkoani Morogoro, Hamis Abdalah Ramadhani, amesema mchakato huo huanza kwa kuloweka mpunga kabla ya kuupitisha kwenye mfumo wa mvuke.
Amesema utaratibu huo husaidia kuimarisha punje za mchele na kupunguza kuvunjika wakati wa kusaga, hivyo kuwezesha kupatikana kwa mchele wenye ubora zaidi na kuongeza thamani ya zao hilo sokoni.






