Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Usultani wa Oman zimeingia makubaliano mapya yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya habari, ikiwemo kubadilishana uzoefu, ujuzi na mafunzo ya kitaaluma kwa waandishi na wataalamu wa vyombo vya habari wa nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa Oktoba 1, 2026, jijini Dar es Salaam, kupitia Jukwaa la Waandishi wa Habari Tanzania na Oman, ambapo pia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesaini makubaliano na Chama cha Waandishi wa Habari Oman kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kitaaluma.
Akifungua jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Abdallah Kilima, amewahimiza waandishi wa habari wa nchi hizo kutumia weledi wao kuandika na kusambaza taarifa sahihi zitakazochangia kuimarisha uhusiano na kuibua fursa kwa mataifa hayo.
Balozi Kilima pia amesisitiza matumizi sahihi ya teknolojia ya akili bandia (AI) katika kuboresha utoaji wa habari na kujenga jamii salama, huku akieleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kutangaza utalii, fursa za uwekezaji na kuhamasisha maadili mema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma, amesema jukwaa hilo limetokana na uhusiano nzuri na wa muda mrefu kati ya Tanzania na Oman na litatoa nafasi kwa wanahabari wa nchi hizo kubadilishana uzoefu na kuongeza ujuzi, sambamba na kukuza ushirikiano katika utalii na uwekezaji.
Jukwaa hilo limehudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Oman, akiwemo Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud bin Hilal Al Shidhani, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Waandishi wa Habari Oman, Dkt. Mohamed Mubarak.
TANZANIA NA OMAN WAINGIA MAKUBALIANO MAPYA KUIMARISHA SEKTA YA HABARI

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Usultani wa Oman zimeingia makubaliano mapya yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya habari, ikiwemo kubadilishana uzoefu, ujuzi na mafunzo ya kitaaluma kwa waandishi na wataalamu wa vyombo vya habari wa nchi hizo mbili.





