Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amekutana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Uswisi na Mkuu wa Kitengo cha Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Nchi zinazozungumza Kifaransa, Balozi Philipp Stalder, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Septemba 30, 2026, yalijikita katika maeneo ya biashara na uwekezaji, maendeleo ya ujuzi, pamoja na ushirikiano wa kitaasisi kati ya nchi hizo mbili.
Balozi Kombo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa fursa za mafunzo na kubadilishana maarifa, huku akieleza haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta binafsi za Tanzania na Uswisi.
Aidha, Waziri Kombo ametaja fursa kwa kampuni na taasisi za kifedha za Uswisi kushiriki katika miradi ya miundombinu inayoiunganisha Tanzania na masoko ya kikanda.
Kwa upande wake, Balozi Stalder amesema Uswisi iko tayari kuwezesha uhusiano kati ya taasisi, vyuo vikuu na wafanyabiashara wa Tanzania na Uswisi, kwa lengo la kuendeleza ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.






