THAMANI ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeongezeka kwa asilimia 16 na kufikia Sh trilioni 11.42 hadi Juni 2026, kutoka Sh trilioni 9.84 zilizorekodiwa Juni 2025.
Kutokana na ukuaji huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, ameitaka menejimenti ya NSSF kuendelea kuboresha huduma kwa wanachama na kuhakikisha zinawafikia wananchi katika maeneo yao, wakiwemo wanaofanya kazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
Dk. Burian ameyasema hayo wakati wa kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja ya NSSF mkoani Tanga, akisisitiza kuwa huduma bora zinapaswa kuonekana kwa vitendo kupitia urahisi wa upatikanaji na kasi ya kushughulikia mahitaji ya wanachama.
Amesema matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kuongeza mawakala katika maeneo ya vijijini, ni miongoni mwa hatua zinazoweza kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za hifadhi ya jamii kwa wananchi wengi zaidi.
Ameongeza kuwa NSSF inapaswa kuzingatia mahitaji tofauti ya wanachama, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara wadogo, wajasiriamali na wafanyakazi wa viwandani, badala ya kuwachukulia kama namba katika mifumo ya utoaji huduma.
Katika hatua nyingine, Dk. Burian ameitaka menejimenti ya NSSF mkoani Tanga kuendelea kuwafuatilia waajiri wanaoshindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili kulinda haki za wanachama.
Amesema zoezi la kuwafuatilia waajiri lililofanyika mwaka juzi liliwezesha kukusanywa kwa Sh milioni 633, hivyo kuitaka timu ya mkoa kuendeleza juhudi hizo kuhakikisha michango inawasilishwa kwa mujibu wa taratibu.
Aidha, amewahimiza waajiri wenye malimbikizo ya michango kutumia fursa ya msamaha wa tozo iliyotolewa na NSSF kabla ya Desemba 31, 2026, ili kurekebisha madeni yao na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao.
Dk. Burian pia ameipongeza NSSF kwa kuboresha mifumo ya ulipaji wa mafao, akibainisha kuwa kupungua kwa muda wa kushughulikia malipo kutoka siku 60 hadi 19 ni hatua muhimu katika kupunguza usumbufu kwa wanachama.
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma za kidijitali ili wanachama waweze kufuatilia michango yao na kuwasilisha madai ya mafao bila kulazimika kutembelea ofisi za mfuko huo.
Vilevile, ameitaja NSSF kuwa miongoni mwa taasisi zilizochangia kuendeleza shughuli za kiwanda cha mkonge cha Sisalana, akisema hatua hiyo imesaidia kulinda ajira za wafanyakazi zaidi ya 1,000.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema mfuko huo utaendelea kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Tanga kuwafikia watu waliojiajiri na wanaofanya shughuli zao katika sekta isiyo rasmi ili nao wanufaike na huduma za hifadhi ya jamii.
Mshomba amesema matumizi ya TEHAMA yamechangia kuboresha utendaji wa mfuko huo, akieleza kuwa muda wa wastani wa kulipa mafao kwa wastaafu umepungua kutoka siku 63 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi siku 19 kwa sasa.
Amesema NSSF itaendelea kuimarisha huduma kwa wateja na kuwataka watumishi wake kuongeza juhudi katika kuhakikisha wanachama wanahudumiwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Aidha, Mshomba amebainisha kuwa thamani ya mfuko huo imeendelea kukua kwa kiwango kikubwa, kutoka Sh trilioni 4.8 Machi 2021 hadi Sh trilioni 11.42 Juni 2026, hali inayoonesha ongezeko la thamani ya mali za mfuko katika kipindi hicho.






