Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, amepongeza uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya chama hicho, ambalo limefikia asilimia 55.
Chatanda amesema jengo hilo linatarajiwa kukamilika Februari 5, 2027, siku ambayo CCM itatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Jengo hilo liliwekewa jiwe la msingi Mei 28, 2025 na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Chatanda amesema mradi huo ni sehemu ya maono ya Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiwataka wasimamizi na wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha jengo linakamilika kabla ya maadhimisho ya miaka 50 ya chama.
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Khamis Juma, amesema viongozi hao wamefurahishwa na kasi ya ujenzi, akieleza kuwa hatua iliyofikiwa inaonyesha kwamba mambo makubwa yanawezekana pale kunapokuwa na dhamira ya pamoja.






