Imeelezwa kuwa vijana wanapaswa kufundishwa namna ya kufanya maamuzi sahihi na kujisimamia wenyewe, ili waweze kutumia teknolojia kwa uangalifu na kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Baadhi ya vijana wamesema ushauri na mwongozo kutoka kwa wazazi ni muhimu katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia, kutokana na wingi wa taarifa na changamoto wanazokutana nazo kupitia mitandao ya kijamii.
Wamesema ushauri wa wazazi unaweza kuwasaidia kuchambua taarifa wanazokutana nazo, kutambua mambo yenye madhara na kufanya maamuzi yatakayowasaidia kufikia malengo yao.
Kwa upande wao, wazazi wameeleza umuhimu wa vijana kuwa na utamaduni wa kuomba ushauri kabla ya kufanya maamuzi muhimu, wakisema uzoefu wa wazazi unaweza kuwasaidia kutambua changamoto na kuepuka makosa katika safari ya maisha.
Mshauri wa Malezi na Familia, Muhere Madam, amesema pamoja na vijana kuhitaji ushauri kutoka kwa wazazi, ni muhimu pia kufundishwa namna ya kufanya maamuzi na kujisimamia wenyewe ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha kwa ufanisi.






