Unguja. Wananchi wa Kijiji cha Uzi Kiswani, Mkoa wa Kusini Unguja, wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga katika fukwe za bahari, wakisema shughuli hiyo inatishia usalama wa makazi yao na mustakabali wa kisiwa chao.
Ombi hilo limetolewa leo, Oktoba 13, 2026, mbele ya Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia ACT Wazalendo, Prof. Omar Fakih Hamad, wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Omar Suleiman alisema uchimbaji huo umeongeza hofu ya maji ya bahari kuingia katika makazi yao. “Hii ni dalili ya kupoteza kisiwa, kwani kila uchao maji ya bahari yanaingia majumbani kwetu kwa sababu ya uchimbaji wa mchanga ufukweni,” alisema.
Wananchi hao walidai kuwa baadhi ya wachimbaji wanaendelea na shughuli hizo kwa baraka za viongozi wa Serikali, wakiwemo wanaohusishwa na kamati za Shehia. Mahadhi Abdulkheiry aliitaka Serikali kuchukua hatua za haraka, akionya kuwa kisiwa cha Uzi kinaweza kutoweka. “Kila unapopita, ufukweni au kwenye makazi yetu, utaona mashimo ya kila aina yanayohatarisha watoto wetu na hata sisi wazee,” alisema.
Marhumi Hemed Suleiman alisema hali hiyo inatia wasiwasi kuhusu usalama wa kisiwa na maisha ya wakazi, akitaka hatua zichukuliwe kabla madhara hayajawa makubwa zaidi.
Uvuvi haribifu na ajira
Wananchi hao pia wameomba kupigwa marufuku kwa uvuvi unaotumia nyavu zinazoharibu mazingira ya baharini, wakisema unachangia uharibifu wa matumbawe na samaki wachanga. Mselemu Ali Fumu alisema uvuvi huo unadhuru viumbe wa baharini na rasilimali wanazozitegemea kiuchumi.
Aidha, walieleza wasiwasi kuhusu upatikanaji wa ajira za Serikali, wakidai kuwa baadhi ya vijana wazawa wa Uzi hukosa fursa. Shamuni Husein Abdallah alisema vijana hao wanastahili fursa sawa na wengine. “Leo wageni ndio wanaonekana na kuthaminiwa kuliko sisi wazaliwa wa hapa. Inauma sana,” alisema.
Wizi wa mazao na utalii
Marhumi Hemed Suleiman pia alilalamikia uharibifu na wizi wa mazao, yakiwemo minazi, mananasi na mihogo, akidai kuwa baadhi ya wahalifu hukata mazao hayo na kuwalishia mifugo yao. Aliiomba Serikali kuongeza nguvu kukabiliana na vitendo hivyo.
Kuhusu utalii, wananchi walisisitiza umuhimu wa kuendeleza utalii unaozingatia sheria, mila na tamaduni za Wazanzibari, wakipinga vitendo wanavyodai vinakiuka maadili ya jamii. “Tusiwaache watalii wanaokwenda uchi na wanaotembeza pombe,” alisema Marhumi.
Is-haka Husein Abdallah, anayejitolea katika utunzaji wa mazingira kisiwani humo, alisema uharibifu wa mikoko, miti ya asili na fukwe unaweza kupunguza mvuto wa utalii na kuathiri uchumi wa eneo hilo. Alisema wananchi wamekuwa wakihifadhi miti ya asili ili kulinda mazingira na kuvutia watalii, akionya kuwa uharibifu huo unaweza kushusha thamani ya utalii wa Uzi.
Bei ya mwani
Katika kilimo cha mwani, wananchi waliwaomba wawakilishi wao kupaza sauti katika Baraza la Wawakilishi ili bei ya zao hilo iongezwe na iendane na gharama za uzalishaji. Subira Abdul Bari aliomba Serikali kuwapatia vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kulima katika maeneo yenye kina kirefu cha maji na kuongeza ubora wa uzalishaji. “Tupatiwe boti zitakazoweza kufika kina kikubwa cha maji,” alisema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Seif Hamad Suleiman, aliwahakikishia wananchi kuwa atawasilisha kero zao katika Baraza la Wawakilishi ili zifanyiwe kazi na kupatiwa ufumbuzi.
Akihitimisha ziara hiyo, Prof. Omar Fakih Hamad aliitaka Serikali kuliangalia kwa karibu hali ya kisiwa cha Uzi, akisisitiza umuhimu wake katika uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii. Aliwahimiza wananchi kushirikiana kulinda rasilimali za kisiwa hicho kwa manufaa yao na taifa, akionya kuwa uharibifu wa mazingira unaweza kuwaathiri wakazi wote.
“Kwa kuwa wachimbaji wa mchanga na wanaokata miti ya asili wanatoka humu humu Uzi, nawaombeni mshirikiane kulinda urithi wenu ambao ni muhimu kwa taifa,” alisema Prof. Omar, akisisitiza umuhimu wa kulinda fukwe, mikoko, miti ya asili na rasilimali nyingine zinazokifanya kisiwa hicho kuwa na thamani ya kipekee.






