Rais wa China, Xi Jinping, amemtaka Rais wa Marekani, Donald Trump, kuwa makini katika kushughulikia suala la Taiwan, akisisitiza umuhimu wa Washington kuheshimu msimamo wa China kuhusu eneo hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la China, Xinhua, Xi amesema China inatarajia Marekani kuendelea kuunga mkono msimamo wa kupinga Taiwan kujitenga na China.
Xi amesema kushughulikia suala la Taiwan kwa umakini ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya China na Marekani.
China inaichukulia Taiwan kuwa sehemu ya eneo lake, licha ya Taiwan kujitawala yenyewe kwa miongo kadhaa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Beijing imeongeza shinikizo la kijeshi na kisiasa dhidi ya Taiwan, ikipinga hatua zozote zinazoweza kuelekea kwenye uhuru rasmi wa kisiwa hicho.
Kwa upande mwingine, Marekani haina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Taiwan, lakini chini ya sheria yake inaendelea kuiunga mkono katika uwezo wa kujilinda.
Washington kwa muda mrefu imekuwa ikifuata sera ya kudumisha uhusiano usio rasmi na Taiwan, huku ikiendelea kuwa na uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Beijing.






